Watoto wawili wameuawa kwa kuchinjwa na mama yao mzazi mkoani Simiyu na kisha mama huyo kujinjinja.
Tukio hilo limetokea leo, Ijumaa Oktoba 22, katika Kijiji cha Lalago wilayani Maswa majira ya saa mbili asubuhi ambapo mama huyo aliwachukua watoto wake wawili na kwenda nao kwa mdogo wake ambaye hata hivyo hakuwepo nyumbani na ndipo alipowachinja watoto wake hao Nseya Kisena aliyekuwa na miaka saba (7) na Majaba Kisena aliyekuwa na mwaka mmoja na nusu na baadae kujichinja mwenyewe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Blasilius Chatanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mama aliyetekeleza tukio hilo ni Ng’washi Makigo aliyekuwa na umri wa miaka 35 ambapo alipofika nyumbani kwa mdogo wake huyo na alipomkosa aliingia ndani na kuanza kuchinja mtoto wake wa kwanza na baadae kumchinja wa pili mwisho alijimalizia mwenyewe kwa kutumia kisu ambacho kilikutwa shingoni kwa mama huyo.
Inaelezwa kuwa mama huyo alikuwa na tatizo la ugonjwa wa akili kwa muda mrefu na miaka ya nyuma aliwahi kufanya jaribio la kujiua kwa kujichana na kisu.
Jeshi la Polisi lilichunguza miili hiyo na kuikabidhi kwa familia kuendelea na taratibu nyingine.