Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetangaza kuanza kwa mgawo wa maji katika Mkoa Dar es Salaam unaosababishwa na upungufu wa maji Mto Ruvu, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam leo na kusema Mamlaka imeandaa utaratibu wa kuhakikisha hakuna Mwananchi anapata shida ya ukosefu wa maji licha ya uwepo wa mgao huo.
“Kwa sasa hali ya Mto Ruvu kwa majuma mawili bado iko palepale ambapo kina cha Mto kiko katika mita 1.5 hadi 1.8, kwa upande wa Ruvu Juu kina kipo mita 16 hadi 18, hivyo hali ya Mto imeendelea kuimarika, kabla ya changamoto ya kiangazi, Mamlaka huwa inazalisha lita Milioni 520 kwa siku, kwa sasa tunazalisha lita Milioni 460 kwa siku, hivyo upungufu wa maji upo kwa asilimia 12″ ——— Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Luhemeja.
Mhandisi Luhemeja ameongeza kuwa kutokana na ukubwa wa mtandao wa DAWASA, Mamlaka imetoa ratiba ya migao wa upatikanaji wa huduma ambazo zitatolewa kwa Wananchi kupitia mifumo ya kimawasiliano ya Mamlaka katika ofisi za Mikoa ya kihuduma——— “Lengo la kuwa na mgao ni kuhakikisha kila Mwananchi anaendelea kupata maji kwa uwiano”
Mtendaji Mkuu amefafanua kuwa maeneo ambayo hayataathirika na mgawo huo ni pamoja na eneo la Kisarawe, Chalinze, Pugu, Bagamoyo, Oysterbay, Masaki, Mikocheni, Ikulu, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Kikwete (JKCI) na Soko Kuu la Kariakoo.