Kiongozi wa waasi anayepambana na wapiganaji wa Serikali, amesema vikosi vyake vipo karibu na Mji Mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, na vinatayarisha mashambulizi mengine, akitabiri kwamba mapigano yatamalizika hivi karibuni huku wanadiplomasia wakiendelea na majadiliano ya kujaribu kusitisha mapigano.
Jaal Marroo, Kamanda wa Jeshi la Ukombozi la Oromo OLA, amemuonya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwamba, wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wanaendelea kuasi na wapiganaji wanaoipinga serikali wanaelekea kuchukua ushindi.
Jeshi la OLA pamoja na washirika wake wa Jeshi la ukombozi wa jimbo la Tigray TPLF katika wiki za hivi karibuni wamedai kupata ushindi kwa kudhibiti baadhi ya miji na hawajaondoa uwezekano wa kuukamata pia mji mkuu, Addis Ababa.
Kitisho cha waasi kuendelea kudhibiti baadhi ya miji kumesababisha mataifa ya kigeni kuendelea kujadili namna za kusitisha mapigano ambayo tayari yamesababisha vifo vya maelfu ya watu.