Madaktari Bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wazawa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (Aorta) uliokuwa umetanuka pamoja na valvu yake (Aortic valve insufficiency) bila ya usimamizi wa madaktari kutoka nje.
Mafanikio hayo yanakuja baada ya miaka kadhaa ya kujifunza upasuaji huo kutoka kwa wataalam wenzao wanaofika JKCI kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
Upasuaji huo unaojulikana kama Bentall Surgery uliochukua saa tano kukamilika. Ulifanyika hivi karibuni ambapo mgonjwa anaendelea vizuri na anatarajia kuruhusiwa wakati wowote kuanzia sasa.
Mgonjwa huyo alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifua na baada ya uchunguzi aligundulika kuwa mshipa mkubwa wa damu (aorta) unaotoa damu kutoka kwenye moyo na kusambaza damu mwili mzima.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Godwin Sharau amesema tatizo hilo mara nyingi huwapata watu wengi wenye umri wa kuanzia miaka ya 50.