Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limekabidhi serikalini mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazogusa sekta ya habari nchini.
Mapendekezo hayo yanagusa sheria na/au baadhi ya vifungu vya sheria ambavyo kwa mtazamo wa wadau wa habari nchini, vinakwaza kwa namna moja au nyingine uandishi wa habari na vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mapendekezo hayo yamepokewa leo (Jumanne Novemba 16, 2021) mjini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji kutoka kwa Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balile amesema Muhtasari uliowasilishwa unalenga kuiwezesha serikali kuzingatia mapendekezo ya wadau wa habari katika mchakato wa marekebisho ya sheria husika, kabla ya kupelekwa bungeni kwa ajili ya kupata baraka za Bunge.
“Sheria zilizochambuliwa katika muunganisho huu ni Sheria ya Huduma za Habari, 2016, Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, 2016 na ile ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta; (Maudhui ya Mtandaoni) Kanuni, 2020 na Sheria ya Uhalifu wa Mtandao, 2015,” Balile.
Alitaja baadhi ya mambo ambayo wadau wanaomba kufanyiwa marekebisho au kubadilishwa katika Sheria hizo kuwa ni pamoja na mamlaka ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambayo inaweza kufungia vyombo vya habari vinapodhaniwa au kutuhumiwa kuwa vimekosea, bila suala au makosa husika kufikishwa katika vyombo vya kisheria vya kiuamuzi kama Mahakama.
“Wadau tunaona kuwa kifungu kama hiki kinamnyima mtuhumiwa nafasi ya kujitetea na kinakiuka kanuni ya msingi ya chombo kusikilizwa kabla kuhukumiwa,” Balile.