Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) amewataka askari wa uhifadhi nchini kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa manufaa ya Taifa.
Ameyasema hayo leo katika kikao chake na Askari Uhifadhi alipotembelea Hifadhi ya Pori la Akiba Kijereshi lililoko Wilayani Busega mkoani Simiyu.
“Niwaombe tufanye kazi kwa uadilifu, uwajibikaji na utii katika kulinda rasilimali za Taifa” Masanja amesisitiza.
Aidha, amekiagiza Kitengo cha Intelijensia kuhakikisha kinasambaratisha mitandao ya ujangili kwa kuzuia mipango yao yote na kutegua mitego ya ujangili ili kuendeleza utalii na pia ameitaka Idara ya utalii wilayani hapo kuweka mipango thabiti ya kukuza na kuendeleza utalii.
Aidha, Masanja amewataka askari hao kushirikiana na wananchi katika kukabiliana na tatizo la tembo.
“Tuwe karibu na wananchi kwa kuwaelimisha namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu na pia inapobidi tuwapatie vifaa vitakavyowasaidia kufukuza wanyama hao ” Masanja.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Maafisa na Askari Uhifadhi kutoka Pori la Akiba Kijereshi na Kikosi dhidi ya Ujangili kutoka Bunda na Mkoa wa Mwanza.