Rais wa Marekani Joe Biden amelifanyia majaribio gari jipya la Hummer linalotumia nishati ya umeme baada ya kutembelea kiwanda cha General Motor huko Detroit na Hamtramck, Michigan, siku ya Jumatano kusherehekea ufunguzi wa kiwanda na kukuza usaidizi wa Serikali kwenye utengenezaji wa magari ya umeme.
Majaribio haya aliyoyafanya Biden ilikuwa ni sehemu ya ziara yake ya kitaifa kutangaza muswada wa miundombinu ya $ 1 trilioni za Biden ambao umetiwa saini na kuwa sheria siku ya Jumatatu, yote hii ni katika kuyapa nguvu makampuni yanayotengeneza magari yanayotumia nishati ya umeme ili kupambana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na magari mengi ya sasa yanayotumia mafuta.
Sheria hii mpya inazitoa dola bilioni 7.5 za ufadhili kwenye kujenga mtandao wa taifa wa kuchaji magari ya umeme, uwekezaji ambao unatarajiwa kuwahamasisha Wamarekani wengi zaidi kununua magari ya umeme na watengenezaji kuyazalisha mengi zaidi ambapo kwa mwaka 2020 uuzaji wa magari ya umeme ulichangia 1.8% tu ya soko la magari mapya la Marekani.