Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni imetupilia mbali kesi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutokana na mapungufu ya kisheria.
Uamuzi huo, umetolewa leo na Hakimu Allon Lyamuya baada ya Upande wa mleta maombi, Saed Kubenea kupitia Wakili wake, Hekima Mwasipu kuomba kuiondoa kesi hiyo kutokana na kukosea baadhi ya sheria wakati wa kuifungua.
Kutokana na hatua hiyo, Wakili Mwasipu amesema wataifungua kesi hiyo tena baada ya kumaliza marekebisho ya vifungu vya sheria ambavyo hakuvitaja.
“Lengo la kuiondoa ni kufanya maboresho kwa sababu ni kesi yenye maslahi mapana kwa taifa, tumepokea maoni kutoka kwa wadau, nadhani hadi Jumatatu inaweza kuwa tayari,” amesema Wakili Hekima.
Kubenea kupitia wakili wake Mwasipu, alimshitaki Makonda katika kesi ya jinai namba 7, ya mwaka 2021 katika tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi ya madaraka. Mbali na Makonda washitakiwa wengine walikuwa ni Mkurugenzi wa Mashitaka na DCI.