Mgombea urais nchini Kenya ameahidi mikopo ya kati ya $4,400 (£3,300) na $8,800 kwa wanandoa wote wapya iwapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi utakaofanyika mwakani.
Gavana wa Machakos Alfred Mutua, ambaye alikuwa akizindua ilani yake ya urais Jumapili, alisema mkopo wa riba ya chini utakaolipwa ndani ya miaka 20 utasaidia familia “kuanza maisha vizuri”.
Vilevile mgombea huyo amesema serikali yake itahimiza upandaji miti na kuhesabiwa kama sehemu ya malipo ya mahari. “Unapoenda kulipa mahari, unapaswa kusema umepanda miti mingapi,” Bw. Mutua alisema wakati wa uzinduzi huo ambao ulitangazwa moja kwa moja kwenye vituo vya televisheni nchini humo.
Lakini ahadi hii imeibua shutuma kali na kejeli kutoka kwa Wakenya mtandaoni.
Takriban wanasiasa 12 tayari wameanza kampeni za kumrithi Rais aliye madarakani Uhuru Kenyatta, ambaye yuko katika miezi ya mwisho ya miaka 10 madarakani.