Vitengo vyote vya kijeshi nchini Marekani vimeanza kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa wake ambao wamekataa chanjo iliyoidhinishwa dhidi ya UVIKO-19, ambapo wanajeshi elfu 20 ambao hawajachanjwa tayari wanakabiliwa na hatari ya kuondolewa kazini.
Mapema jana Desemba 16, kitengo cha jeshi la wanamaji kilisema kimewasimamisha kazi maafisa wake 103 hadi sasa kwa kukataa chanjo hiyo, huku jeshi la nchi kavu likiwachukulia hatua za kinidhamu zaidi ya wanajeshi 2,700 na kusema litaanza mchakato wa kuwaachisha kazi mwezi Januari mwakani.
Mapema wiki hii, jeshi la anga lilisema kuwa wanajeshi wake 27 waliachishwa kazi kwa kukataa kutii agizo hilo la kupata chanjo ambapo kwa miezi kadhaa sasa, uongozi wa jeshi umekuwa ukitahadharisha kwamba wanajeshi watachukuliwa hatua iwapo hawatafuata kile kinachochukuliwa kuwa agizo la kupata chanjo hiyo.