Kenya imesitisha safari zote za ndege za abiria zinazoingia na kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ili kulipiza kisasi hatua ya Dubai ya kupiga marufuku safari zote za ndege za abiria kutoka Kenya kutokana na vipimo bandia ya Covid-19.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (KCAA) Gilbert Kibe ameliambia gazeti la The EastAfrican siku ya Jumanne kwamba kusimamishwa huko kulianza Jumatatu usiku wa manane kwa muda wa siku saba.
Marufuku hiyo hata hivyo haiathiri safari za ndege za mizigo ambazo kwa kawaida husafirishwa na wachukuzi kama vile Kenya Airways na shirika la ndege la Emirates kutoka UEA hadi Kenya.
“Safari za ndege za abiria za ndani na nje kutoka UAE zimesitishwa kwa muda wa siku saba. Tunafanya hivi ili kujibu marufuku ya safari za ndege za abiria za Kenya kuelekea UAE,” Kibe.
Marufuku hiyo inajiri siku chache tu baada ya UAE kuongeza muda wa marufuku ya safari za ndege nchini Kenya baada ya kubaini kuwa wasafiri kutoka Nairobi walipimwa na kukutwa na Covid-19 baada ya kuwasili katika taifa hilo la Mashariki ya Kati, licha ya kuwa na matokeo yaliyoonyesha kwamba hawakuwa na virusi vya Covid.