Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wametoa Pole kwa wafanyabiashara wa soko la Karume kwa kuunguliwa na mali zao leo Januari 16, 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala amefikisha salamu hizo kwa wafanyabiashara wa soko la Michikichini Karume na kusema kuwa Viongozi wa nchi wanawasihi wawe na uvumilivu na kutopeana maneno ya uongo wakisubiri uchunguzi kukamilika.
Amesema kuanzia Mida ya saa 9 usiku wahusika wa uzimaji wa moto wamejitahidi kudhibiti moto ili usienee katika makazi ya wananchi na kutokana na miundombinu ya soko hilo ugumu ulionekana ingawa kazi kubwa imefanyika.
“Mpaka sasa hivi chanzo cha moto hakijajulikana ijapokuwa tunaambiwa ulianzia kwa mama lishe, ingawa pia tunaskia kuna wafanyabiashara walikua wanajiunganishia umeme kinyemela, lakini hatuwezi kusema kama ndio chanzo,”
“Baada ya timu ya uchunguzi ambayo nimeiteua ambayo itaanza kazi kesho, inajumuisha Jeshi la zimamoto na uokoaji, TANESCO, ofisi ya Mkurugenzi, ofisi ya mkuu wa wilaya na Jeshi la Polisi, wanafanya uchunguzi kwa siku 14 na hapo ndipo tunaqeza kusema chanzo ni nini,” alisema.
Msemaji wa wafanyabiashara ndogo ndogo ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, Masoud Issa, amewasihi wafanyabiashara wote ambao wamepata madhara katika eneo hilo wawe watulivu wakisubiri maamuzi ya Serikali na namna watakavyosaidiwa kupata maeneo mengine ya kuendelea na biashara zao kwa sasa wakati ukarabati utakapokua unafanyika.
“Na sisi tunazidi kuishauri Serikali kuwa haya majanga yanatokea mara kwa mara, haya ndio maeneo yetu ambayo tunatafutia riziki, tunaishauri serikali watujengee mfumo ambao hata Zimamoto inaweza kuingia na kufanya kazi kwa haraka. Wafanyabiashara nawaomba tuwe watulivu ili tuisikilize serikali ikifanya kazi yake na siis viongozi tuko nayo karibu,” alisema Masoud.
Hata hivyo mpaka asubuhi hii magari na vikosi vya zimamoto bado vimeendelea katika juhudi za kuzima moto huo na kuokoa vitu vichache ambavyo vimenusurika