Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji ameitaka Tume ya Ushindani (FCC) kutoa sababu za kuadimika kwa vinywaji baridi sokoni pamoja na kupanda bila utaratibu kwa bei ya vifaa vya ujenzi.
Akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo Dk. Kijaji amesema kwa siku za karibuni kumekuwepo na kuadimika kwa vinywaji baridi hali iliyopandisha bei ya bidhaa hiyo.
“Hivi ni kweli tunasubiri mwezi mzima soda zinapotea, bei inaanza kupanda ndiyo tunakuja, hii siyo sawa hivyo naomba ndani ya siku tatu nipate taarifa ya kwanini soda zimeadimika ndani ya soko la Taifa letu” Dk. Kijaji
“Lakini ndani ya siku Saba pia nipate taarifa ya sababu za kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi ili tuwambie watanzania kuwa bei halisi unayopaswa kununua nondo ni hii na bei halisi unayopaswa kununua saruji ni hii, hatupangi bei maana ni uchumi wa soko huria lakini tunafanya utafiti kwa manufaa ya wananchi wetu” Dk. Kijaji
Ni wajibu wa Tume ya Ushindani kutuambia nini kimesababisha bei ya vifaa vya ujenzi ipande na sasa bei ya vinywaji baridi nayo imepanda baada ya kuadimika kwa muda, ni lazima FCC mtuambie sababu za kupanda huko.