Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, amezindua mradi wa ushirkiano kati ya wasindikaji na wazalishaji wa maziwa wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 47.
Mradi wa TI3P ni wazo mama la Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation na unalenga kuondoa changamoto iliyopo katika sekta ya mifugo na maziwa nchini, ukilenga kuwafikia wafugaji 100,000 na viwanda kati ya 9 na 12.
Taasisi ya Bill & Mellinda Gates Foundation ya nchini Marekani, imetoa ruzuku ya Dola za Kimarekani Milioni 7, sawa na shilingi bilioni 16.2 za kitanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo huku Serikali kupitia TADB ikiongezea Dola milioni 40.
Akizindua mradi huo, Waziri Mkuu alisema mradi huo utaongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, ukusanyaji wa maziwa katika mfumo ulio rasmi, kukuza uwezo wa viwanda katika uchakataji wa maziwa, na kupanua wigo wa soko la bidhaa za maziwa.
“Tanzania imeendelea kuwa muagizaji mkubwa wa maziwa kutoka nje ya nchi, huku zikitumika angalau shilingi bilioni 15 kwa mwaka. Kiwango hiki cha fedha ni kikubwa ikilinganishwa na fursa iliyopo katika sekta ya maziwa nchini,” Mhe Majaliwa alisema.
Licha ya kushika nafasi ya pili kwa idadi ya mifugo Barani Afrika, sekta ya mifugo inachagia asilimia 7.4 tu kwenye Pato la Taifa. Kwa sasa, sekta ndogo ya maziwa inachangia asilimia 2.3 ya pato la taifa, na inakua kwa wastani wa asilimia 5 tu kwa mwaka. Pia uzalishaji wa maziwa umeongezeka kwa kiwango kidogo kutoka lita bilioni 2.1 mwaka 2016, hadi kufikia lita bilino 3.1 mwaka 2021.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji ta TADB Frank Nyabundege alisema “Mradi huu wa TI3P ambao tunaingia katika makubaliano leo na taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation unalenga kupandisha mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la kupitia uhamasishaji wa uwekezaji kutoka sekta ya umma na sekta binafsi ili kuongeza pato la Taifa kwa maendeleo ya Taifa letu”,
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, Serikali imekubali kufanikisha kiasi cha dola milioni 40 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya uwekezaji katika mradi huo, huku taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation ikitoa msaada wa kiasi cha dola milioni 7.
“Tayari fedha hizo zimeshafika nchini kwa ajili ya kuanza rasmi kazi ya kuleta mageuzi kwa wasindikaji na wazalishaji katika tasnia ya maziwa nchini,’ Bw Nyabundege alisema.
Alibainisha kuanzia mwaka 2018 hadi tarehe 28, Februari 2022, TADB katika sekta ya maziwa pekee imewekeza shilingi bilioni 16.4 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 15.6 kimekopeshwa moja kwa moja kwa wafugaji na viwanda vya maziwa katika mikoa ya Arusha, Dare s salaam, Iringa, Mara, Njombe, Tanga na Shinyanga.
Mkuu wa mkoa wa Tanga Adam Malima alisema mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji na tija kwa sekta ndogo ya maziwa katika mkoa wake ikiwa ni pamoja na kuboresha hali ya kiuchumi kwa wafugaji na mkoa kwa ujumla.