SHAHIDI wa 6 katika kesi ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kumiliki genge la uhalifu inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake sita, Watson Mwahomange (27), amedai katika maisha yake akiwa na Sabaya amefanya kazi katika mateso makubwa na alikuwa kama mateka.
Mwahomange ambaye wakili wake, Fridorini Bwemelo alijitoa kumtetea, alidai hayo wakati akijitetea mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda na kusema kuwa anamfahamu Sabaya tangu mwaka 2019.
Alidai kuwa Januari 22 mwaka jana, Sabaya na walinzi wake walienda katika gereji ya mfanyabiashara Francis Mroso, huku shahidi huyo akiwa chini ya ulinzi, ikiwa ni pamoja na kufungwa pingu, baada ya kipigo kutoka kwa walinzi wake kwa amri yake.