Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema Urusi imeshindwa kupata udhibiti wa anga la Ukraine hadi sasa ikiwa ni karibu wiki ya nne toka ianze mashambulizi ambapo kushindwa huko kupata udhibiti ni moja ya sababu za vita yake kukosa mafanikio ambayo iliyatarajia ndani ya muda mfupi.
Taarifa za leo za kijasusi kutoka Wizara ya ulinzi ya Uingereza zimesema Urusi imeshindwa kupata udhibiti wa anga na kwa kiasi kikubwa na kuifanya ibaki kutegemea kufanya mashambulizi yake ya anga kutokea kwenye anga la Urusi.
Imefahamika kwamba lengo la Urusi kwenye Nchi ya Ukraine lilikua ni kuifikia Ikulu ya Nchi hiyo ndani ya siku mbili tu za mwanzo lakini hadi sasa hilo halijawezekana kutokana na uimara wa Jeshi la Ukraine na jinsi walivyoweza kuwadhibiti Wanajeshi wa Urusi ambapo pia kupata udhibiti wa anga la Ukraine ilikua ni moja ya malengo muhimu ya kufanikisha kwenye siku za mwanzo.