Ujerumani imechukua umiliki wa tawi la kampuni kubwa ya nishati inayomilikiwa na serikali ya Urusi Gazprom nchini humo.
Mdhibiti wa nishati wa Berlin atasimamia kampuni hiyo kwa muda licha ya msisitizo wa hapo awali wa Moscow kwamba hatua kama hiyo itakuwa kinyume cha sheria.
Gazprom Germania, kampuni tanzu ya Gazprom yenye makao yake mjini Saint Petersburg, inaendesha baadhi ya vituo vikubwa zaidi vya kuhifadhi gesi asilia nchini Ujerumani.
Waziri wa Uchumi Robert Habeck alitangaza uamuzi huo siku ya Jumatatu, akisema (uamuzi huo) utamaanisha kwamba miundombinu ya nishati ya Ujerumani “haiko chini ya maamuzi ya Kremlin.”
“Mpangilio wa utawala wa uaminifu unatumika kulinda usalama na utulivu wa umma na kudumisha usalama wa usambazaji,” Habeck aliwaambia waandishi wa habari, na kuongeza kuwa hatua hiyo “ni muhimu na haraka” ili kuhakikisha “usalama wa usambazaji nishati nchini Ujerumani.”
Ujerumani inakabiliwa na upungufu mkubwa wa nishati ya mafuta na gesi asilia na imekuwa ikitegemea bidhaa hiyo kutoka Urusi. Hata hivyo kutokana na mzozo wa Ukraine na vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi, Moscow ilitangaza kuwa haitaruhusu gesi yake kuendelea katika mataifa yasiyo rafiki ikiwemo Ujerumani ikiwa watashindwa kununua kwa sarafu yake ya ruble.