Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla ametoa siku Saba za Uchunguzi wa chanzo Cha Kuvuja kwa Mafuta Ghafi Bandarini na kusababisha athari za kimazingira.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kukagua Miundombinu ya mafuta Kigamboni ambapo amesema Baada ya kukamilika kwa Uchunguzi hatua za kisheria zitachukuliwa.
Aidha RC Makalla amesema Kamati ya Uchunguzi wa chanzo hicho itajumuisha Kamati ya Ulinzi na usalama, TRA, Waagizaji wa Mafuta kwa pamoja, NEMC na Wadau wengine.
Katika ziara hiyo RC Makalla pia ametembelea Ghala la kuhifadhi Mabaki ya mafuta taka la TAZAMA lililoteketea kwa moto juzi ambapo ameelekeza kusimama kwa Shughuli zote za uchakataji Mafuta yaliyoganda mpaka pale watakapopata maelekezo kutoka Baraza la usimamizi wa Mazingira NEMC.
RC Makalla amesema taarifa ya NEMC inaonyesha kuwa TAZAMA walishapewa onyo kuhusu Ufanyaji wa Shughuli hiyo kwenye eneo Hilo Kutokana na kuwepo kwa Makazi ya Wananchi jambo ambalo ni hatari kiusalama lakini Cha kushangaza Shughuli zimekuwa zikifanyika pasipo uwepo wa Vifaa vya kudhibiti moto.
Kwa mujibu wa taarifa zinaeleza kuwa chanzo Cha Moto huo kilitokana msuguano wa kitu kinachodhaniwa kuwa ni Jiwe/Chuma kilichozalisha cheche na kusababisha moto Kutokana na zoezi lililokuwa likiendelea la kulainisha Mabaki ya mafuta taka yaliyoganda.
Hata hivyo RC Makalla ametembelea na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Kituo Cha Afya Somangila kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 250 kupitia fedha zilizotokana na Tozo za Simu na kukamilika kwake kutasaidia upatikanaji wa huduma Bora za Afya kwa zaidi ya Wakazi 35,000 ambapo RC Makalla ameonyesha kuridhishwa na hatua za Ujenzi.