Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya amezindua kampeni ya Msichana Wetu (Our Girl) yenye lengo la kukata mnyororo wa umasikini, mila potofu zinazosababisha Wasichana kuolewa katika umri mdogo, kupata mimba za utotoni na kukatiza masomo mapema.
Kampeni hiyo ambayo inagharimu Tsh. Milioni 190 tayari imepata ufadhili wa Taasisi ya kujitegemea ya Solidermed iliyopo Ulanga ambayo imeshatoa fedha hizo ili kufanikisha Walengwa kufikiwa.
“Malengo yetu mengine kupitia kampeni hii ni kupunguza makali ya kiuchumi kwenye Familia zenye Watoto wa kike kwa kutambulisha mpango wa kuwezesha Jamii kibiashara kwa makubaliano ya kufikia lengo maalum la kijamii, Jamii kuongezewa uelewa kuhusiana na masuala ya usawa wa kijinsia, elimu ya uzazi kwa Vijana na haki za Wanawake, kuongeza ustawi wa Familia kwa kupunguza unyanyasaji wa kijinsia na ushiriki mzuri wa Wanawake katika maamuzi na kupunguza kuvunjika kwa ndoa pia matokeo chanya kwenye afya ya Mama na Mtoto”
“Tunatarajia kupitia kampeni hii Watoto wa kike watabaki shuleni kwa kupunguza utoro/kuacha Shule, tutapunguza ndo za lazima katika umri mdogo hasa zinazochangiwa na umasikini, tutapunguza mimba katika umri mdogo, kuongeza kipato cha Familia ili kujikimu katika kukidhi mahitaji ya Mtoto wa kike Shuleni na pia kuwa na moduli ya biashara/ujasiriamali na masoko ambayo itawezesha Waelimishaki Jamii na Kaya kuongeza kipato”