Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amesema chanzo cha moto uliopelekea kuteketea kwa Soko la Veterinary lililopo TAZARA Wilaya ya Temeke ni hitilafu ya umeme.
RC Makalla amesema hayo alipotembelea soko hilo kujionea uharibifu wa mali zilizoteketea moto ambapo amesema taarifa za awali zinaonyesha moto huo umeathiri vibanda 453.
RC Makalla amesema Serikali inafanya taratibu za haraka kuhakikisha kazi ya kurejesha miundombinu iliyoharibika inafanyika usiku na mchana ili Wafanyabiashara warudi kuendelea na biashara na kuahidi kwamba hakuna Mfanyabiashara atakaeondolewa.
RC Makalla ametoa pole kwa Wafanyabiashara walioathiriwa na moto huo na kuwataka kuwa watulivu wakati Serikali yao inaendelea kutatua changamoto hiyo.
Kutokana na matukio ya moto kujirudia mara kwa mara, RC Makalla ameendelea kutoa wito kwa Viongozi wa masoko kuhakikisha kila soko linakuwa na fundi umeme anaetambuliwa na TANESCO, Halmashauri kuweka vifaa vya kudhibiti moto kwenye kila soko na Wafanyabiashara waache tabia ya kuhinjika maharage jioni ili asubuhi wakute yameiva na pia kutaka masoko yawe na ulinzi.