Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki (EASTC) kimezindua awamu ya pili ya mafunzo ya kidigitali yatayowawezesha wasimamizi wa Sensa ya nyumba na makazi kutumia vifaa vya kidigitali hususani vishikwambi katika kutekeleza zoezi la sensa linalotegemewa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Ahmed Mohammed Ammy amesema kuwa mafunzo hayo ni ya pili kutolewa ambapo awali wasimamizi wa zoezi la sensa walifundishwa kuhusu suala la maudhui ya sensa na hivyo kwa sasa kutokana na mabadiliko ya teknolojia wameona ni vyema kutoa elimu juu ya matumizi ya vifaa vya kidigitali katika kuendesha zoezi hilo.
Aidha Mwenyekiti wa bodi ameongeza kuwa zoezi la Sensa kwa mwaka huu halitohusisha idadi ya watu pekee lakini pia takwimu za makazi zitahusika hivyo zoezi hilo halitofanyika kwa muda wa siku moja kama ambavyo imezoeleka kwa sensa zilizopita.
Mafunzo hayo ya awamu ya pili yanafanyika kwa muda wa wiki moja yakihusisha takribani washiriki 119 kutoka mikoa mbalimbali ambapo baada ya mafunzo kuisha kunategemewa kufanyika mafunzo mengine kwa yatayofanyika kwa muda wa siku mbili jijini Dodoma.