Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe Balozi Dkt Pindi Chana amewapongeza waratibu wote na wananchi wa Ngorogoro walioamua kuhamia Kijiji Cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Tanga, kwa uratibu mzuri wa watu na mifugo yao hali iliyopelekea wafike salama.
Waziri Balozi Dkt Chana ameyasema hayo kijiijini Msomera Tanga baada ya kujihakikishia kuwa mifugo ya wafugaji hao kutoka Ngorogoro imefika salama.
“Tunamshuku Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutuongoza vyema kwenye jambo hili, limeenda vizuri na linaenda vizuri kwa Wanagorogoro wenyewe kuhama kwa hiyari, sisi kama Wizara tutaendela kutekeleza maagizo ya Viongozi wetu wa juu ili kuhakikisha ndugu zetu wanaishi kwenye Mazingira Bora kama mlivyo yaona”. Waziri Balozi Chana
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa ambaye aliungana na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwan Kikwete kupokea jumla ya kaya 20 kati ya 290 zilizowasili Msomera, Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga zilizoamua kuondoka kwa hiyari katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Waziri Bashungwa amesema, tayari Serikali imeweka mazingira mazuri kwa ajili yao ambapo Serikali ilileta shilingi Milioni 400 kujenga shule mpya za msingi na sekondari na bweni moja katika Kata ya Misima ndani ya Kijiji cha Msomera ambazo zimekamilika ili wanafunzi wasitembee mwendo mrefu kupata masomo ya elimu ya msingi na sekondari.
Amesema, tayari Serikali imetoa shilingi Milioni 500 kuanza ujenzi wa kituo cha afya Msomera ambao unaendelea na shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kupanua na kuboresha huduma za afya katika zahanati ya Kijiji cha Msomera katika kata ya Misima Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga kinachotoa huduma kwa wananchi wasiopungua 10,000.
Bashungwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaongeza watumishi ambao ni wauguzi, wataalam wa maabara na madawa ili ukarabati unaofanyika katika zahanati ya Msomera uendane na huduma nzuri zinazoendelea kutolewa hapo.
Amesema kuwa TARURA wanaendelea wa barabara inayotoka Handeni Mjini hadi Kata ya Misima kwa kujenga makalavati na boksi kalvati katika maeneo korofi.
Pia, amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuleta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa awali ili yaweze kuwahudumia watoto wadogo walio katika eneo la Msomera.
Akizungumzia hali ya Usalama ya Wafugaji hao, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Adam Malima, amesema wanachi hao wapo salama na wataendelea kuwa salama wao na mifugo yao hivyo Serikali ya Mkoa imejipanga vyema kuwahudumia vizuri kwa kuwa wamesha kuwa wakazi wa Tanga.
Naye Waziri wa Maji Mhe Juma Aweso amesema miradi ya maji imesha fanyika na wanaendelea kuhakikisha hakutokuwa na changamoto yeyote ya maji kwa Matumizi ya binadamu na ya kunywesha mifugo iliyofika na itakayo fika.