Mahakama Kuu imemruhusu Halima Mdee na wenzake 18 Wabunge waliovuliwa uanachama na CHADEMA kufungua shauri la kupinga uamuzi wa Chama hicho kuwavua uanachama huo.
Uamuzi huo umetolewa leo baada ya Mahakama hiyo kukubaliana na hoja za maombi yao ya ridhaa ya kufungua shauri hilo la kupinga kuvuliwa uanachama.
Maombi hayo ya kina Mdee yalisikilizwa mbele ya Jaji Mustapha Ismail Juni 30, 2022 ambapo CHADEMA kupitia kwa jopo la Mawakili wake linaloongozwa na Peter Kibatala, walipinga hoja za Mawakili wa kina Mdee kuwa hazikidhi matakwa ya kisheria kupewa ruhusa hiyo.
Hata hivyo Jaji Ismail katika uamuzi wake amekubaliana na vigezo na hoja zote za kina Mdee, zilizowasilishwa na Mawakili wao, Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu.
Kutokana na hatua hiyo, Mdee na wenzake wanatakiwa kufungua shauri lao hilo ndani ya siku 14 kuanzia leo.