Baada ya Changamoto ya miaka mingi ya kukosa maji safi na salama kwa Wananchi wa Kijiji cha Nakafuru kata ya Lupiro wilayani Ulanga sasa mambo safi.
Wananchi hao walimuomba mbunge wa Jimbo hilo awatatulie Changamoto hiyo kwani ni adha kubwa jambo linalopelekea kina mama na watoto kuteseka kufuata maji kwa umbali mrefu na wakati mwingine kunywa maji yasiyo salama jambo linalohatarisha maisha yao kwani Afya zao zinakuwa matatani.
Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mhe SALIM ALAUDIN HASHAM baada ya kusikia kilio hicho akatoa kiasi cha Shilingi Milioni 2.5 kwaajili ya uchimbaji wa visima vitano na utengenezaji wa miundombinu ya bomba ili maji yapatikane kwa uhakika bila changamoto.
Zoezi la uchimbaji wa visima limekamilika na mapema katibu wa mbunge wa jimbo hilo Ndugu Thomas Justice Daffa amewakabidhi wananchi visima hivyo na kuwataka wavitumie kwa umakini kwa kuvitunza ili viwasaidie kwa muda mrefu.
Visima hivyo vilivyochimbwa na kampuni ya Msabi pia vitakuwa na utaratibu wa kufanyiwa matengenezo mara kwa mara na kampuni hiyo ili kuhakikisha wananchi wa eneo hilo hawakosi maji safi na salama wakati wote.
Baada ya kukabidhiwa visima hivyo wananchi wa eneo hilo walimshukuru Mbunge kwa msaada huo mkubwa kwani kilio hicho kilikuwa cha miaka mingi na walimuomba aendelee na moyo hio wakuwasikiliza Wananchi wake na kuwatatulia changamoto zao zinazowakabili.