Kufuatia makubaliano baina ya wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) tuzo za ubora zilianzishwa ili kutambua na kukuza sekta ya biashara kupitia ubora wa bidhaa na huduma katika ukanda huu. Washiriki wa Tuzo za ubora za SADC wanapaswa watokane na washindi wa tuzo za ubora za kitaifa.
Ameyasema hayo leo Julai 14,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Bw.Christopher Mramba kwenye hafla ya Utoaji wa Tuzo za kitaifa za Ubora kwa washindi wa mwaka 2021/2022.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara iliona umuhimu wa kuanzisha Tuzo za ubora za Kitaifa na kutoa jukumu la kuziratibu kwa Shirika la Viwango Tanzania pamoja na TPSF.
“Tuzo hizi ni sehemu ya mipango ya serikali katika kuboresha huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini kupitia matumizi ya viwango na kanuni za ubora kwa taasisi za umma na sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa mifumo, bidhaa na huduma zinakidhi mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa na hivyo kufanya vizuri kwenye masoko ya ngazi zote hizo”. Amesema Bw.Mramba.
Aidha amesema washindi wa tuzo hizo watapata fursa ya kushiriki kwenye mashindano ya tuzo za ubora kwa Nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya maendeleo kwa Nchi kusini mwa Afrika (SADC) na hivyo kupata nafasi ya kufahamika na kupata masoko zaidi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw.David Ndibalema amesema Katika zama hizi tulizopo ni ngumu kuzuia bidhaa na huduma kutoka kwenye nchi moja kuuzwa kwenye nchi nyingine kutokana na uwepo wa kanuni za kimataifa hususani kanuni za WTO zinazozuia kuweka vikwazo vya kiufundi kwenye biashara yaani WTO Technical Barrier to Trade Agreement.
“Kwa sababu hiyo njia bora ya kulinda soko la bidhaa na huduma zetu ndani na nje ya mipaka yetu ni kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu”. Amesema Bw.Ndibalema.
Amesema wazalishaji na watoa huduma wanahitajika kujengewa au kujijengea utamaduni wa ubora na ushindani hapa nchini. Vilevile wanahitaji kufahamu uhusiano kati ya ubora na ushindani. Hii ndiyo njia pekee kwa nchi yetu kusonga mbele kibiashara, hasa katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.
Pamoja na hayo amesema moja ya hatua zilizochukuliwa serikali yetu ili kujenga utamaduni wa kuthamini ubora kwenye jamii yetu ni kuanzisha tuzo za kitaifa za ubora.
“Tuzo hizi zinafanyika ikiwa ni msimu wa pili zikiwa na lengo la kuwatambua na kuwapongeza watu binafsi pamoja na taasisi zinazofanya vizuri kwenye masuala ya ubora wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za uzalishaji bidhaa au utoaji huduma. Lengo jingine kufanyika kwa tuzo hizi ni kuhamasisha ubunifu na uboreshaji wa bidhaa na huduma zinazotolewa hapa nchini kupitia taratibu zilizowekwa chini ya miundombinu ya ubora”. Amesema