Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy amewafuta kazi watumishi 28 wa shirika la ujasusi la nchi hiyo, SBU, siku moja baada ya kumfungisha virago mkuu wa masuala ya ujasusi, Ivan Bakanov.
Katika hotuba yake kwa taifa ya kila jioni, Zelenskiy amesema kuwa waliofukuzwa wanatoka katika ngazi mbali mbali za shirika hilo, na kuongeza kuwa kwa ujumla, sababu za wao kuondolewa ni zile zile, kutokuwa na ufanisi wa kutosha kazini.
Hivi karibuni rais huyo alielezea kufadhaishwa kwake na ukweli kuwa mawakala zaidi ya 60 wa kijasusi na wale kutoka ofisi ya mwendeshamashitaka mkuu wa Ukraine wamesalia katika maeneo yaliyokamatwa na Urusi, kitendo ambacho serikali yake inakichukulia kama uhaini.
Mwendeshamashitaka mkuu Iryna Venediktova pia ameachishwa kazi.