Mkoa wa Manyara unatajwa kuwa kwa sasa una jumla ya idadi ya watu millioni moja, laki nane na elfu sabini na tano sawa na ongezeko la asilimia 3.2.
Hayo yamesemwa na mkuu wa Mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere leo katika kongamano la wiki ya maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani ambalo limekutanisha makundi mbalimbali ya watu na Viongozi kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Kwa upande wake Mchambuzi wa masuala ya idadi ya watu na maendeleo kutoka shirika la Umoja wa mataifa la idadi ya watu (UNFPA) Ramadhani Hangwa amesema muda wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka kutoka wastani wa miaka 61 hadi miaka 66 mwaka 2022 ambapo amesema uboreshwaji wa huduma za kijamii ikiwemo Afya na Maji ni miongoni mwa sababu za ongezeko hilo.
Siku ya Idadi ya watu Duniani kwa Tanzania itaadhimisha Julai 20,2022 katika viwanja vya shule ya Msingi Katesh B Wilayani Hanan’g mkoani Manyara ambapo kumetanguliwa na kongamano maalum la kujadili fursa na changamoto za ongezeko la idadi ya watu Duniani.
Nae Kamishna wa tume ya Mipango Zanzibar Salma Makame amesema Suala la ongezeko la idadi ya watu hapa Tanzania ni baraka na kwamba kupitia Uchumi wa Blue wameshaandaa mpango maalum wa Kilimo halisi kwa ajili ya vijana.
Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu “Dunia ya watu Bilioni nane kuhimili wakati ujao ni fursa ya haki kwa wote,shiriki Sensa kwa maendeleo endelevu”