Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ameeleza kuwa Serikali haipeleki umeme vijijini kwa ajili ya kuwasha taa pekee bali kuchagiza pia shughuli za kiuchumi ikiwemo uanzishaji wa viwanda.
Amesema hayo baada ya kutembelea kiwanda kinachochakata parachichi ili kutengeneza mafuta cha KUZA AFRIKA kilichopo wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya mbacho kimeunganishiwa umeme na TANESCO.
Makamba amesema kuwa, uwepo wa Kiwanda hicho ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya Nishati ambao umezaa matunda kwani kiwanda hicho pamoja na kuongezea thamani mazao ya Wakulima, kimezalisha ajira zaidi ya 200 ndani ya kiwanda na katika mashamba ya parachichi.
Ameongeza kuwa, msingi mzima wa kupeleka umeme vijijini ni kusawazisha maendeleo kati ya watu wa vijijini na mijini kwani shughuli za kiuchumi kama za viwanda zinaboresha pia uchumi wa wananchi wa vijijini.
Meneja wa TANESCO, Wilaya ya Rungwe, Mhandisi Mukhsin Kijemkuu amesema kiwanda hicho kabla ya kufungiwa transforma yake kilikuwa kikizalisha lita 2000 kwa siku lakini baada ya kupata Transfoma wiki moja iliyopita kitazalisha lita 4000 kwa siku.
Ameongeza kuwa kwa lita 4000 zinazotarajiwa kuzalishwa kwenye kiwanda hicho mwekezaji angetumia shilingi milioni 50 kununua dizeli ya kuendesha mitambo ila kwa kuwa sasa anapata umeme wa kutosha atatumia takriban shilingi milioni 30.
Pamoja na kuishukuru Wizara ya Nishati kwa kutenga fedha za kupeleka umeme kwenye maeneo kama hayo amekaribisha wawekezaji wengine kuwekeza kwenye miradi kama hiyo kwani hali ya upatikanaji umeme sasa imeimarika na pia TANESCO Itaongeza mapato yake.