Waziri wa Nishati, Mhe January Makamba ametoa ufumbuzi wa changamoto ya muda mrefu ya mgawo wa umeme wa masaa 12 kwa vijiji 20 vilivyopo Wilaya ya Ludewa ambavyo vimekuwa vikipata umeme kutoka kampuni ya Madope inayoendesha mradi huo mdogo wa umeme wa maji (MW 1.7) ambayo inaundwa na wadau mbalimbali wakiwemo Jumuiya ya Watumia Umeme Lugarawa na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
Imeelezwa kuwa changamoto hiyo ya mgawo wa umeme imetokana na waya unaotumika kusambaza umeme kuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji ya Wananchi ambao wanaotumia umeme kwa shughuli za kiuchumi kama vile kuendesha mashine za kukamulia alizeti na kukoboa na kusaga nafaka.
Mbele ya Wananchi wa Kijiji cha Lugarawa, Waziri Makamba amesema kuwa >>‘Serikali kupitia TANESCO imeamua kununua umeme wote unaozalishwa na kampuni hii baada ya kufanya mazungumzo na wadau wote wanaohusika na mradi huu pamoja na TANESCO ili kuwezesha Wananchi kupata umeme wa uhakika kwani kwa sasa katika megawati 1.7 zinazozalishwa, umeme unaotumika ni 0.3 na pia kampuni hii ya Madope itapata mapato’ – Waziri Makamba.
Makamba ameongeza kuwa >> ‘Wataalam wa TANESCO watafika hapa Lugarawa tarehe 7 Agosti 2022 ili kufanya tathmini ya Miundombinu ya Usafirishaji umeme pamoja na kusaini mikataba ya makubaliano hayo na inategemewa kuwa ifikapo mwezi wa Pili mwaka 2023 wananchi wote wa Ludea mtaku mmeshaanza kupata umeme wa uhakika’ – Waziri Makamba.
Mradi huo wenye wateja 3200 kwa sasa umeleta manufaa mbalimbali kwa Wananchi wa Kijiji hicho ikiwemo kutoa huduma ya umeme katika vituo vya afya, shule za Sekondari 5, shule za msingi 19 na kituo kimoja cha kulelea watoto yatima.
Utekekelezaji wa Mradi wa umeme wa Madope umewezeshwa na wadau mbalimbali ikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao ulitoa shilingi Bilioni 4.5 kuendeleza mradi huo.
WAZIRI MAKAMBA ALIVYOMPIGIA SIMU WAZIRI BASHE MKUTANONI KUTATUA CHANGAMOTO