Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza kwamba Kiongozi wa Kundi la Al-Qaida, Ayman al-Zawahiri, ameuawa na mashambulizi ya ndege yasiyo rubani ya Marekani mjini Kabul, nchini Afghanistan, huku Saudi Arabia.
Akizungumzia kutokea Ikulu ya White House usiku wa kuamkia Jumanne (2 Agosti), Biden aliitaja operesheni iliyomuua Zawahiri mjini Kabul kwamba imetenda haki na italeta faraja kwa familia za Wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.
Mbali ya mashambulizi hayo ya Septemba 11, Biden ametumia sababu nyingine ya ziada kuhalalisha uamuzi wake wa kuamuru mauaji ya Zawahiri “Alifanya video, zikiwemo za wiki za hivi karibuni, akiwataka Wafuasi wake kuishambulia Marekani na Washirika wetu, sasa haki imetendeka na Kiongozi huyu wa kigaidi hayupo tena”
Akielezea undani wa mashambulizi hayo ya ndege zisizo rubani yalivyofanyika, Biden amesema Maafisa wa ujasusi wa nchi yake waliifuatilia nyumba ya Zawahiri katika mtaa mmoja wa Kabul, ambako alikuwa akijificha na familia yake, na baadaye yeye Biden akaidhinisha operesheni hiyo wiki iliyopita na ikatekelezwa juzi Jumapili.
“Operesheni hii ilipangwa kwa uangalifu, na kwa kiwango kikubwa imepunguza madhara kwa raia wengine, Wiki moja iliyopita, baada ya kushauriwa kwamba mazingira yalikuwa sahihi, nilitoa idhini ya mwisho ya kumpata, na operesheni imefanikiwa, hakuna hata Mtu mmoja wa familia yake aliyeumizwa na hakuna madhara yoyote kwa raia”