Watumishi wa kada mbalimbali katika Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi ambazo anazifanya hasa kuwajali watumishi na kuzingatia maslahi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 3,2022 Jijini Dar es Salaam,Mtumishi wa Wilaya ya Temeke Bi.Makungu Shomari amesema kuwa Rais Samia ndani ya kipindi chake cha muda mfupi ameweza kuleta nafuu na faraja kwa watumishi wa Umma.
“Kuhusu suala la nyongeza ya asilimia 23 sisi watumishi tumelielewa sana mana lengo kuu Rais Samia amezingatia kuboresha Hali za kiuchumi za watumishi wa kiwango cha chini ambao ni wengi zaidi katika kada mbalimbali za utumishi wa umma, hapa amezingatia wenye viwango vidogo vya mishahara”. Amesema Bi.Makungu
Aidha amesema kuwa Rais Samia amejipambanua kuwa anawajali watumishi sana na kwa kuzingatia maslahi yao na alianza kwa kuwaondolea kadhia ya watumishi wenye deni la mkopo wa elimu ya juu,
“Rais Samia alipoingia madarakani alifuta penati hii na imeleta ahueeni kubwa na Sasa Deni linalipika, baada ya mabadiliko hayo aliyekuwa analipa milioni 8 Sasa analipa milioni 4 pekee.”Amesema
Pamoja na hayo amesema kuwa suala la posho na nauli amesema Rais Samia ameongeza kiwango kwa asilimia 100 na hii imeleta ahueni kwa watumishi wanapopewa kazi maalumu.