Waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Kenya kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wametoa ripoti yao ya awali inayoonesha kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa uwazi.
Akitoa ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Nairobi, Kenya, kiongozi wa waangalizi hao Dkt. Jakaya KIkwete amesema kampeni za uchaguzi huo zilifanyika kwa uhuru na kama kulikuwa na dosari basi ni ndogo tu.
Dkt. Kikwete ambaye ni Rais mstaafu wa Tanzania amesema kabla na siku ya upigaji kura ulinzi uliimarishwa, na kwamba vikosi vya Kenya vilitekeleza majukumu yao kwa ufanisi pasipo kuleta usumbufu kwa wapiga kura.
Amevipongeza vikosi hivyo vya Kenya kwa kufanya kazi na kuendelea kufanya kazi kwa weledi.
Dkt. Kikwete ameongeza kuwa, matumizi ya TEHAMA yamesaidia uchaguzi huo mkuu wa Kenya kuwa wa uwazi zaidi, hali ambayo pia imesaidia kupunguza malalamiko.
Kwa watendaji mbalimbali waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi huo Dkt. Kikwete amesema, wengi ni wenye uwezo mkubwa na ambao wanafahamu watekeleze vipi majukumu yao kwa ufanisi.
Waangalizi hao wa uchaguzi mkuu wa Kenya kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wameipongeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kwa kuandaa uchaguzi mzuri ambao umefanyika katika mazingira ya uhuru, uwazi na haki.