Chuo kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo ( SUA) kilichopo Mkoani Morogoro wamezindua kigoda kinachojulikana kama Oliver Tambo ambacho kinajihusisha na kufanya tafiti ya Magonjwa ya virusi vya Wanyama na Binadamu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa kigoda hicho Profesa Gerald Misinzo amesema kuwa lengo la kigoda hicho ni kufanya tafiti za Magonjwa yatokanayo na virusi vya wanyama na bindamu ili magonjwa hayo yaweze kupata tiba.
Profesa Misinzo amesema katika programu hiyo wamepata kiasi Cha Shilingi bilioni 2.3 ili kutekeleza shughuli hiyo kwa kipindi Cha miaka mitano.
Profesa Misinzo amesema njia moja wapo itakayotumika katika kutekeleza tafiti hizo ni pamoja na utekelezaji wa Afya moja kwa sekta ya Afya mifugo na sekta ya afya ya binadamu kushirikiana katika Utendaji kazi pamoja.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Omary Kipanga amesema Serikali inahakikisha tafiti zinazofanywa zinaleta tija kwa kutatua changamoto katika jamii.
Mhe. Kipanga amesema kumekua na tafiti nyingi ambazo zinafanywa na baadhi ya Vyuo lakini zinaishia kwenye makabati Jambo ambalo halina faida.
Amesema Serikali imeongeza fedha za utafiti kutoka bilioni 3 hadi bilioni 9 ili kuviwezesha vyuo vinavyofanya tafiti ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na Magonjwa mbalimbali.