Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imepokea, kujadili na kushauri taarifa ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kiutendaji ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa TBA, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Suleiman Kakoso ametoa pongezi na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Wakala huo.
Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa miradi yenu, ila hakikisheni mnaweka mikakati inayotekelezeka kwani uwekezaji kwenye ujenzi wa nyumba unakuwa wa kubadilika kila siku hivyo mnatakiwa muende sambamba na mabadiliko hayo ili kuweza kupata wateja ndani na nje ya nchi, amesema Kakoso.
Aidha, Mhe. Kakoso ameitaka TBA kuhakikisha inaendelea kubuni miradi mbalimbali katika maeneo ambayo wanamiliki ili kulinda maeneo yao pamoja na kusambaza huduma kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesisitiza TBA kuendelea kuwa wabunifu kwa kuhakikisha inaendelea kujenga na kukarabati nyumba na majengo ya Serikali ili kuongeza ubora wa makazi kwa viongozi na watumishi wa umma.
Waziri Mbarawa ameitaja miradi mikubwa ya kitaifa ambayo imetekelezwa na TBA kuwa ni ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota, jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Sekou-Toure Mwanza, jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Ujenzi wa makazi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Usimamizi wa mradi wa ujenzi wa Ikulu Chamwino Dodoma.