Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imeridhishwa na Ubunifu, Ujenzi na Usimamizi wa miradi ya ujenzi wa majengo ya Serikali ambayo yanatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) baada ya kufanya ziara ya kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na TBA Mkoani Dodoma.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ulipo eneo la Medeli, mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za viongozi katika eneo la Kisasa na mradi wa ujenzi nyumba 3500 unaotekelezwa katika eneo la Nzuguni.
Akizungumza baada ya kuona utekelezaji wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Jerry Slaa amesema Kamati imeridhishwa na utekelezaji mzuri wa miradi hiyo.
“Kamati ya Bunge imeridhika na kazi iliyofanyika ni kubwa na nzuri, tunachotaka tu ni kuongeza kasi na weledi katika kazi, na sisi kama Kamati wakati wowote tutawasaidia katika kufanikisha kutekeleza miradi yenu” amesisitiza Mwenyekiti Jerry Slaa.
Aidha, Kamati imeipongeza TBA kwa kubuni majengo mazuri na kutekeleza ujenzi kwa viwango bora na kushauri kuanza kutekeleza miradi yake kwa kushirikiana na Sekta binafsi kwa njia ya ubia.
Mradi mwingine mkubwa ambao Kamati pia imepongeza ni ujenzi wa mji wa Serikali, unaojengwa eneo la Mtumba Jijini Dodoma. Katika mradi huo TBA, imefanya ubunifu wa majengo ya Wizara 24 na Taasisi nne za Serikali zinazojengwa katika mji huo. Vile vile TBA inajenga jengo la ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Vile vile Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imepongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kuwashirikisha wataalamu vijana kusimamia miradi mikubwa ya ujenzi inayotekelezwa na TBA katika sehemu mbalimbali nchini. Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na TBA mkoani Dodoma.
“Kitu kikubwa tulichojifunza katika ziara yetu ni usimamizi na shughuli nyingi kufanywa na vijana kwenye miradi hii ya ujenzi inayofanywa na TBA, wasanifu majengo walioko kwenye miradi hii ni vijana, wahandisi ni vijana, watu wa stoo ni vijana, hivyo tumewaasa na wenyewe kujenga ile dhana ya vijana kulitumikia Taifa lao kwa uzalendo” Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Jerry Slaa.
Katika hatua nyingine Kamati imepongeza hatua ya TBA kuthamini suala la jinsia katika miradi yake kwa kuwapa nafasi vijana wa kike kusimamia miradi, hatua hiyo inasaidia kuongeza nguvu kwa watoto wa kike kupenda masomo ya Sayansi.
Awali akifanya wasilisho la miradi mbalimbali inayotekeleza nchini, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, alibainisha kuwa TBA imeendelea kuwa na ubunifu katika kutekeleza miradi yake, huku akitolea mfano ubunifu uliofanyika katika ujenzi wa nyumba 20 za viongozi eneo la Kisasa Dodoma.
“Tuliona nyumba za awali zilizopo zina maeneo makubwa, hivyo tukaona ni bora tukate baadhi ya maeneo yake na kupata viwanja vikubwa ambavyo vimetosha sisi kujenga nyumba hizo, hii ni sehemu mojawapo ya ubunifu tunaofanya kama Wakala” anabainisha Mtendaji Kondoro.