Tanzania itakuwa kitovu cha maunganisho wa mawasiliano Afrika Mashariki na Kati kufuatia uwepo wa mkongo wa mawasiliano wa 2 Afrika utakapokamilika mwakani mwezi februari.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Jimmy Yonazi alipofanya ukaguzi wa mkongo wa kituo cha 2 Afrika Septemba 9, 2022 na kueleza kuwa hilo linafanyika kutokana na juhudi za Serikali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha maunganisho ya mawasiliano.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho unafaida kubwa kwa nchi yetu kwa kupata mtandao wa Intaneti yenye kasi zaidi na uhakika wa kuunganishwa duniani.
“Mkongo unaokuja unapitia kusini mwa bara la Afrka, kwahiyo tutapata uhakika wa maunganisho kwenda duniani na kusaidia sana biashara ya kuuza capacity nchini mwetu na nchi Jirani na kuwasaidia wananchi wetu na nchi Jirani kuweza kushiriki katika uchumi wa kidigitali ambao ndio uchumi sasa dunia inashiriki” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masuala ya Udhibiti na Ushirika Bi Beatrice Singano amesema wanatengeneza eneo la kusambaza mawasiliano yanayopitia baharini (Sea Cable Services) ili kuiwezesha Tanzania kufikiwa na kufikia maeneo mengine kimawasiliano.
Bi Singano ameeleza kuwa, mkongo huo unatokea Djibouti na unahimili kwa kiwango kikubwa uwezo wa kutoa mawasilano tofauti na hapo awali na kuiwezesha Tanzania kukua kimawsiliano na huduma hiyo itanufaisha pia nchi Jirani.
Mkongo huo mpya wa kisasa utakaotoa mawasiliano ya kasi ya hali ya juu kiasi cha terabytes 180 TB ni mmoja kati ya mkongo mkubwa duniani utakao tokea bara la ulaya na kukatiza mashariki ya kati kwa kupitia nchi mbalimbali za Afrika hadi nchini Tanzania.
Mkongo wa 2Africa Submarine unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2023 kwa kufika katika Zaidi ya maeneo 35 katika nchi 26 Duniani.