Jeshi la Polisi mkoani Arusha limewakamata watuhumiwa 38 wanaojihusisha a matukio mbalimbali ya uhalifu ambapo mmoja kati yao amekutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kwa lori la mafuta.
Akitoa taarifa hiyo leo Septemba 11, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika operesheni iliyofanyika kuanzia Septemba 05 hadi Septemba 10, 2022 ikiongozwa na Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha.
Kamanda Masejo amesema kuwa tarehe 10.09.2022 muda wa saa 12:30 asubuhi huko katika mtaa wa Kikwe uliopo katika kata ya Kikwe wilayani Arumeru, Jeshi hilo la Polisi lilimkamata mtu mmoja aitwaye Allen Wilbard Kasamu (49) dereva na mkazi wa Sue Jijini Arusha akiwa anasafirisha madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni mirungi yenye uzito wa zaidi ya kilo 390.75.