Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Jenerali (Mstaafu) George Waitara amepokea ripoti ya operesheni iliyofanikiwa kukamata Mifugo zaidi ya 200,000 iliyovamia Bonde la Ihefu lililopo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mkoani Iringa.
Waitara amepokea ripoti hiyo wakati Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ilipofanya ziara ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Akipokea taarifa hiyo, Mwenyekiti Waitara alisema “ leo tumejionea uvamizi mkubwa wa mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha. Ikumbukwe hifadhi hizi ni mali yetu sote watanzania na ni sehemu ya uchumi wa Tanzania, wakati mifugo ni mali ya mtu mmoja mmoja. Hivyo ni jukumu letu kulinda hifadhi ambayo ni ya Watanzania wote kwa faida ya sasa na ya baadaye”
Aidha, Jenerali Waitara aliongeza kuwa mifugo itakuwa chanzo cha kufa kwa hifadhi zetu, kwani inaua mifumo ya Ikolojia na kusababisha kutoweka kwa wanyama na mimea, hivyo ni muhimu hifadhi hizi zikalindwa kufa na kupona.
Naye Prof. Wineaster Anderson ambae ni mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo, alisema TANAPA ina wajibu mkubwa wa kulinda maliasili zilizomo hifadhini kwa faida ya Watanzania wote. “Tuna wajibu mkubwa katika Taifa hili wa kulinda maliasili hizi pamoja na miradi ya kimkakati kama Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere ambalo linategemea maji kutoka vyanzo vilivyomo hifadhini Ruaha. Kiasi kikubwa cha fedha kimekwishatumika kujenga bwawa hilo na wananchi wana mategemeo makubwa ya kunufaika nalo. Hivyo sisi tukishindwa kulinda hivi vyanzo vya maji tutadaiwa na Watanzania sio tu leo, bali hata baada ya maisha yetu hapa duniani” aliongeza Profesa Wineaster.
Kwa upande wake Mjumbe mwingine wa Bodi, Kamishna wa Polisi Nsato Marijani, alisisitiza kuongeza nguvu katika kufanya doria na kuendeleza operesheni ya kuwaondoa wavamizi wote katika eneo la hifadhi hiyo.
Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema aliishukuru Bodi ya Wadhamini kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha kujionea changamoto kubwa ya uvamizi wa mifugo ambayo ni tishio kwa uhifadhi nchini. Alibainisha kuwa endapo hapatakua na juhudi madhubuti na za dhati za kudhibiti mifugo, itapelekea kufa kwa hifadhi zetu ambazo ni tunu kwa Taifa, na zimekuwa zikituletea fedha, sifa na fahari ndani na nje ya nchi yetu.