Wizara ya Afya, imesema hadi sasa hakuna Mgonjwa wa Ebola nchini Tanzania huku ikiwashauri Wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kugusa mwili au majimaji ya mwili wa Mhisiwa au Mgonjwa wa Ebola na kuepuka safari zisizo za lazima kutembelea maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huu.
Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel ametoa taarifa leo ambapo amesema “Sept 20, 2022 Wizara ilipata taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari juu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda, taarifa ilieleza Mgonjwa aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa Ebola amefariki Wilayani Mubende nchini Uganda”- Naibu Waziri wa Afya Godwin Mollel
“Taarifa hizo zilionesha kuwa na dalili za homa kali, degedege, kutapika matapishi yenye damu, kuharisha na kutokwa damu machoni, taarifa za uchunguzi zinaonesha ugonjwa huu umesababishwa na kirusi cha Ebola aina ya Sudan (Ebola-Sudan strain), uwepo wa ugonjwa huu katika nchi jirani unaiweka nchi yetu katika hatari kutokana na mwingiliano mkubwa wa Watu kupitia mipaka ya nchi kavu, Viwanja vya Ndege na Bandari”- Naibu Waziri wa Afya Godwin Mollel
“Dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni na machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi, ugonjwa huu unaenea kwa kugusa majimaji ya mwili wa mgonjwa mfano mate, damu, mkojo na machozi, endapo utapata au kuona Mtu mwenye dalili hizi, unashauriwa kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya mapema”- Naibu Waziri wa Afya Godwin Mollel