Mkuu wa wilaya ya Mkinga, kanali Maulid Surumbu amewataka Wananchi wilayani humo kuzikataa Taasisi za kijamii zinazokwenda kinyume na mila, desturi na taratibu za wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya, wakati wa kufungua mradi wa kuhamasisha uwajibikaji wa wananchi katika kulinda rasilimali za umma,Mwenyekitiwahalmashauri ya Mkinga, AMANI KASINYA amesema kuwa ni vema wananchi kuwa na uelewa na miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao hususani kutoka kwenye Taasisi zisizo za kiserikali zinazopaswa kuwa wazi katika kutekeleza miradi yao.
“Ni lazima wananchi kuwa na uelewa ili kuifahamu baadhi ya miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao na kuzikataa vikali baadhi ya Taasisi za
kijamii zinazoenda kinyume na taratibu na mila na desturi za wananchi “ alisema Kasinya
Aidha KASINYA amesema mradi huo wa TIMIZA WAJIBU, MWANANCHI SHIRIKI KATIKA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UMMA ni vizuri sasa kwa washiriki kushirikiana kikamilifu kutekeleza mradi huo kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga uelewa kwa wananchi juu ya kubaini changamoto mbalimbali zilizopo kwenye huduma ya afya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa halmashauri ya Mkinga, amesema mradi huo wa kufuatilia rasilimali za umma katika sekta ya afya utawasaidia serikali kubaini
changamoto mbalimbali zilizopo kwenye vituo vya afya na kufikisha kwenye mamlaka husika ili kupatiwa ufumbuzi na kuboreshwa.
Aidha Mkurugenzi wa shirika la WOMEN FOR SELF INITIATIVES (TAWSEI), Bernadetha Choma amesema lengo kuu la mradi ni kuwezesha wananchi kutambua
haki zao za kikatiba, kisheria na kikanuni ili kushiriki uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Aidha Bernadetha amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kwenye kata tatu za Marimba, Daluni na Gombero katika wilaya hiyo ya Mkinga ambapo itasaidia
katika kuamsha ari kwa wananchi katika kuchangia kwenye miradi ya maendeleo.