WANANCHI wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam wameshauriwa kujenga utamaduni wa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabani kama hatua mojawapo ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza hasa kipindi hiki ambacho nchi jirani ya Uganda Kuna tishio la ugonjwa wa Ebola.
Ushauri huo umetolewa leo na Ofisa Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo alipokuwa akipokea msaada wa katoni 11 za sabuni ambazo ni sawa na lita 220 zilizotolewa na Shirika la WaterAid Tanzania kwa lengo la kukabiliana na tishio la Ebola.
Ayo alisema pia msaada huo umekuja wakati muafaka kwani Oktoba 15 ya wiki hii ni Wiki ya kuadhimisha Siku ya Unawaji Mikono Duniani n katika kuadhimisha Siku hiyo wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo WaterAid ambao wamekuwa wakifadhili siku ya Unawaji mikono.
“Wakati tunaelekea Oktoba 15 ambayo ni Siku ya kuadhimisha Unawaji Mikono Duniani niendelee kutoa mwito kwa wadau wengine waendelee kuisaidia jamii kwenye unawaji mikono kwasaabbu jamii inahitaji kunawa mikono,”alisema.
Aliongeza tunafahamu tumetoka kwenye janga la COVID-19 lakini sasa kuna tishio la Ebola ambalo linatishia nchi ya Uganda na kama inavyoeleka nchi hiyo iko jirani na Dar es Salaam ambayo ni kitovu cha biashara,hivyo kuna ndege nyingi zinaingia kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Uganda.
“Kwa hiyo wananchi wote tunatakiwa kuwa na usafi wa mikono na tunaponawa mikono sio tu inazudia COVID- 19 bali inazuia na magonjwa mengine ya kuhara, kipindupindu na magonjwa mengine.
Kauli mbiu ya katika maadhimisho ya mwaka huu inasema mikono salama kwa kila mmoja.
“Kwa hiyo tuungane kuhakikisha kila mmoja anakuwa na mikono safi ili kuepusha kupata magonjwa au kuambukiza magonjwa kwa wengine , kwa hiyo kuelekea siku hii ya unawaji mikono Mkoa wa Dar es Salaam tumehakikisha kila kituo cha afya ,kila zahanati, kila taasisi kunakuwa na maeneo ya kunawa mikono kwa ajili ya kujikinga na maradhi,”alisema.
Wakati huo huo Kaimu Mganga Mkuu Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwananyamala Dk.Aileen Barongo alisema wanashukuru kwa msaada ambao wameupata kutoka Shirika la WaterAid na kwamba wao wanaendelea kuhamasisha watu kunawa mikono.
“Kwa hospitali ya Mwananyamala watu wanaofika hapo wamekuwa wakinawa mikono na kuna vituo vya kutosha watu kunawa mikono.Hata hivyo tunaendelea kuhamasisha watu kujenga utamaduni wa kunawa mikono kwa hiyari badala ya kushurutishwa”– alisema.
Aidha alisema wanatoa shukrani kwa Shirika la WaterAid kwa kuendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kunawa mikono huku akiomba Shirika hilo kuendelea kusaidia lakini pia wanatamani kuona wadau wengine wakijitokeza kujenga vituo vya kunawia mikono.