Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hasaan Oktoba 16 2022, amezindua mradi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme mkubwa wa 220kV/33kV cha Nyakanazi mkoani Kagera ambao umekamilika.
Aidha, Mheshimiwa Rais amezindua maeneo manne ya mradi huo ambayo ni; Njia ya umeme msongo wa kilovoti 220 kutoka Geita mpaka Nyakanazi yenye urefu wa Kilomita 144, Kituo cha Kupoza umeme cha Nyakanazi kutoka kilovoti 220 mpaka kilovoti 33 na matoleo yake sita, Njia ya kwanza inayopeleka umeme wa Gridi ya Taifa mkoani Kigoma kupitia Kibondo hadi Kasulu pamoja na Njia ya kupokea umeme mkubwa wa kilovoti 220 kutoka Rusumo yenye urefu wa Kilomita 94.
Mradi huu wa Nyakanazi una manufaa makubwa kwa Taifa letu, kwani baada ya kukamilika kwa mradi huu, sasa maeneo ya Chato, Biharamuro na Ngara ambayo yalikuwa yanapata umeme mdogo na kutumia majenereta, sasa yanaanza kupata Umeme wa kutosha na wa uhakika, hivyo kustawisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Vilevile kukamilika kwa mradi huu kunaifanya TANESCO kuzima majenereta ya Biharamuro, Ngara, Kibondo na Kasulu hivyo kuokoa gharama kubwa kwa shirika letu la Umeme TANESCO na fedha hizo kuweza kutumika katika maeneo mengine.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja, majenereta yaliyozimwa yatawezesha TANESCO kupunguza gharama za mafuta na matengenezo zaidi ya bilioni 60 za kitanzania.
Pamoja na kuokoa fedha hizo, mradi huu pia utasaidia usalama wa nishati ya umeme kwa kupokea umeme kutoka kituo cha kufua umeme cha Rusumo pale kitakapokamilika mwakani pamoja na kupeleka umeme wa Gridi ya Taifa Bukoba kupitia Benaco hadi Kyaka pamoja na migodi ya Kabanga.
Pamoja na uzinduzi huu, Mheshimiwa Rais ameweka jiwe la msingi wa kituo cha kukuza umeme cha Nyakanazi kutoka kilovoti 220 hadi kilovoti 440 pamoja na Njia kubwa ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa Kilomita 280 ya kutoka Nyakanazi hadi Kigoma.
Mradi huu ukikamilika mwishoni mwa mwaka 2023 utanufaisha mkoa wa Kigoma ambao uchumi wake unakuwa kwa kasi na mahitaji ya umeme yanategemewa kuongezeka na pia kufungua fursa ya kusafirisha umeme kwenda nchi jirani.Miradi yote hii inagharimu takriban shilingi bilioni 600 za kitanzania, na inagharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na fedha za mikopo kutoka kwa African Developement Bank (AfDB), Agence Francaise de Development (AFD) pamoja na Korea Economic Development Co-operation (EDCF).