Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imeitaka Menejimenti ya TANAPA kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha moto katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa zoezi la kukabiliana na moto huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Jenerali (Mstaafu). George Waitara alisema
“Pamoja na kupambana na moto mhakikishe mnafanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto ili kuona matukio haya hayajirudii tena na kuchukua hatua stahiki.” alisema Waitara.
“Tunauthamini mlima huu na jukumu letu wote ni kuulinda kwa namna yoyote bila hivyo eneo hili lote litaathirika sana. Kwa taifa letu Mlima Kilimanjaro ni muhimu sana na ni lazima uwe salama kwa namna yoyote ile.”
Naye, Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, William Mwakilema alibainisha kuwa kinachofanyika sasa ni juhudi za kudhibiti moto pamoja na kuchunguza kwa kina chanzo cha moto ili tukio kama hili lisijirudie tena.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi – Dkt.Maurus Msuha ambaye pia ni Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini alipongeza ushirikiano mzuri uliopo baina ya TANAPA na wadau wengine alisema
“Kama TANAPA wasingekuwa na mahusiano mazuri na wadau wengine hasa wa sekta binafsi ni dhahiri kuwa zoezi hili lingekuwa gumu sana hivyo kufanikiwa kwa kiasi hiki ni ishara ya mahusiano mazuri na wadau hawa.” alisema Dkt. Msuha.
Bodi ya Wadhamini – TANAPA imefanya ukaguzi wa zoezi la uzimaji moto katika Mlima Kilimanjaro na kupongeza juhudi zinazoendelea kufanyika katika kupambana na moto huo.