Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu katika Kitengo cha Huduma za Ajira, kimeendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Maendeleo kuhusu kuongeza fursa za ajira kwa watanzania.
Kitengo hicho kinawezesha watanzania kunufaika na fursa za ajira za staha ndani na nje ya nchi.
Kwa sasa vijana 500 wenye ujuzi wa chini, wa kati na wa juu wataenda kufanya kazi katika Kampuni ya Almarai nchini Saudi Arabia inayojishughulisha na Uchinjaji wa nyama na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo. Jitihada hizo zimefanywa na Kampuni ya Almarai, Mshirika wake kwa upande wa Tanzania Kampuni ya Bravo Job Center Ltd, Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, pamoja na Serikali ya Saudi Arabia kupitia Wizara inayohusika na masuala ya kazi na ajira.
Akiongea wakati wa kuwaanga vijana 50 wa awamu ya kwanza kwenda nchini Saudia, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu, amebainisha kuwa kazi wanazoenda kufanya vijana hao zimezingatia viwango vya msingi vya kazi za staha. Aidha, amewataka watanzania wanaotaka kufanya kazi nje ya nchi kuhakikisha wanaunganishwa kwenye kazi na Mawakala Binafsi wa Huduma za ajira waliosajiliwa na Serikali.
“Kwa sasa tunao mawakala 32 walio sajiliwa nchini, lengo ni kuhakikisha ajira, usalama na haki za msingi za mtanzania zinazingatiwa ili watanzania waweze kufanya kazi zenye viwango vya kazi za staha vinavyokubalika kimataifa na tumeandaa Mwongozo maalum unaosimamia shughuli za Mawakala pamoja na uendeshaji wa shughuli za kuunganisha watanzania na fursa za ajira ndani na nje ya nchi”
Katibu Mkuu aliongeza kuwa kwa sasa Ofisi hiyo imefanya mazungumzo na nchi takribani saba. Aidha, ameongeza kuwa serikali itaendelea kushughulikia michakato ya kazi pamoja na fursa zitakazoendelea kujitokeza katika Mashirikiano ya kibiashara baina ya nchi ya Tanzania na mataifa mengine ikiwemo makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara na mataifa mbalimbali duniani ambayo mara nyingi huambatana na uhamaji wa mitaji pamoja na nguvukazi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ubalozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Fahad Alharbi alifafanua kuwa anayoimani na watanzania kwa kuwa wanazo sifa na ujuzi stahiki unaohitajika wa kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuongeza tija kwenye maeneo ya kazi. nchini Saudi Arabia. Aidha, aliongeza kuwa ubunifu na uaminifu wa watanzania ni mambo ambayo yanaisukuma nchi hiyo kuendelea kutoa fursa za ajira.
Awali akiongea katika mkutano huo Mwakilishi wa Kampuni ya Bravo Job Center Ltd, Abbas Mtevu aliishukuru serikali ya Awamu ya Sita inayoonozwa na Mhe. Rais Samia, kwa kuendelea kuwawezesha watanzania kupata fursa za ajira nje ya nchi. Aidha, amesisitiza kuwa Kampuni yake ambayo ni Wakala wa Huduma za jira nchini itaendelea kuzingatia sheria na miongozo ya kazi na Ajira nchini ili viwango vya msingi vya kazi za staha vizingatiwe.
Naye Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati,Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Hemed Mgaza alibainisha kuwa pamoja na Ubalozi wa Tanzania huko Saudi Arabia na Balozi zingine kuwa kwa sasa zimeweka jambo la kutafuta fursa za ajira za staha kwa watanzania kuwa sehemu ya shughuli za kibalozi kwenye maeneo yao ya uwakilishi.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Nganga alisisitiza kuwa Mawakala wote wa huduma za ajira hawanabudi kuzingatia kuwa uunganishaji wa Watanzania unaongozwa na Sheria ya Kukuza Huduma za Ajira ya mwaka 1999 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2014. Hivyo aliwataka kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia matakwa ya sheria, kanunini pamoja na miongozo ambapo aliahidi kuendelea kushirikiana na nao hasa kwenye nchi za kimkakati kusaka fursa za ajira kwa ajili ya Watanzania.