HALMASHAURI ya Jiji la Tanga kwa kushirikiana na wadau wa Usalama Barabarani wamezindua Mpango wa Safari Salama na Endelevu kwa Jiji hilo lengo likiwa ni kuwa mikakati endelevu wa kuendelea kupunguza ajali za barabarani huku ikielezwa takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2021 zaidi ya asilimia 30 ya watu wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani , hivyo kupoteza nguvu ngazi ya Taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango huo Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hasheem Mgandilwa ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba , alisema mpango huo umelenga kupunguza ajali za barabara hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2025 ambao unafadhiliwa na taasisi ya Amend kwa ufadhili wa Botnar foundation.
Alifafanua kuwa ajali za barabara zimekuwa zikisababisha nchi kuingia gharama kubwa kwa ajili ya kutibu majeruhi wanaotokana nanajali hizo huku familia zikiingia kwenye utegemezi jambo ambalo wakati mwingine hupelekea athari za kiuchumi kwenye ngazi ya familia hadi jamii.
“Mpango Kazi wa Safari Salama na Endelevu unakwenda kupunguza changamoto za ajali, hivyo niwaombe Shirika la Amend kwa kushirikina na Jeshi la Polisi pamoja na wadau wengine wanaohusika na miundombinu ya barabara zetu kuendelea kutoa elimu ya usalama barabara kwa wananchi sambamba na watumiaji wa vyombo vya moto kuheshimu alama za barabara sambamba na madhara ya kuhujumu miundombinu hiyo,”alisema Mgandiliwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo amesema Mpango Kazi huu umeanisha mikakati 10 ambayo imekubaliwa na wadau, na fedha za utekelezaji zimekwisha ainishwa hivyo utekelezaji wake umekwishaanza Mikakati ambayo imeanishwa ni pamoja na kampeni ya usalama barabarani kwa umma kupitia vyombo vya habari.
Pia kuwashirikisha wanasiasa kwenye masuala la usalama barabarani, kuwashirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye kufikisha ujumbe wa usalama barabarani kwa jamii, kuhamasisha uboreshaji wa miundombinu salama ya watembea kwa miguu kwenye maeneo ya shule, kuanzisha na kusimamia maeneo salama ya shule, kuimarisha elimu ya usalama barabarani mashuleni.
Aidha kuhakikisha njia za watembea kwa miguu zipo wazi bila kutumiwa na wafanyabiashara, wajasiriamali, bodaboda na magari, kutoa mafunzo kwa madereva wa pikipiki, kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza mashuleni na kwa waendesha bodaboda, pia kuimarisha ushiriki wa wadau wengine.