Waziri wa habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, Mhe. Nape Moses Nnauye amesema serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, inaendelea kufanya tathmini ya mapitio ya gharama halisi za utoaji wa huduma za mawasiliano nchini ili kuboresha mahusiano yaliyopo baina ya watoa huduma za mitandao ya simu na watumiaji wake.
Waziri Nape amesema kuwa kufuatia kuwepo kwa malalamiko mengi juu ya kupanda kwa gharama za huduma za mawasiliano kwa wateja, serikali imechukua hatua ya kuthibiti mabadiliko yoyote ya ongezeko la gharama za bando katika kipindi ambacho tathimini hiyo inaendelea kufanyika mpaka kukamilika kwake.