Ripoti ya Kidunia ya hali ya ugonjwa wa UKIMWI kwa mwaka 2022 imebainisha kuwa tangu mwaka 2010 maambukizi ya VVU yamepungua kwa asilimia 62 kwa Watu wenye umri wa miaka 15-49 wanaoishi katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, na asilimia 58 kwa Ukanda wa Afrika ya Magharibi.
Ripoti hiyo imezinduliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Ukimwi (UNAIDS) pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Desemba 01 ambayo Kitaifa yatafanyika Mkoani Lindi.
Hafla ya Uzinduzi wa Ripoti hiyo imeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Utawala George Simbachawene, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel Mkurugenzi Mtendaji UNAIDS Bi. Winnie Byanyima pamoja na Watendaji wa Taasisi zinazoshughulika na masuala ya UKIMWI.