Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema kuanzia sasa Serikali itaanza kuzitazama ajira za Vyuo Vikuu ambapo badala ya kuangalia ubora wa ufaulu (GPA) pekee, sasa Watu wataajiriwa kwa kupimwa uwezo wao kwa kufanya usaili akisisitiza kuwa GPA pekee haitoshi.
“Kuangalia ufaulu pekee wa Wanafunzi haitoshi kuboresha elimu badala yake ni muhimu kuongeza vigezo hivyo katika mapitio ya sera na mabadiliko ya mitaala, hilo litatazamwa kwa weledi mkubwa”- amesema.
Profesa Mkenda ameyasema haya leo tarehe 12 December 2022 mbele ya Mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Philiph Moango wakati wa mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Amesema wakati Serikali ikiongeza udahili wa Wanafunzi haitokuwa tayari kuona ubora unapungua hivyo inaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha ubora wa elimu hususani katika Vyuo Vikuu unaimarika.
“Zamani ilikuwa rahisi kuwa Profesa ukiandika tu kwenye magazeti unakuwa Profesa lakini kwa sasa vigezo vya kuwa Profesa vimezidi kuwa vigumu kwa sababu tunataka Maprofesa wetu wawe sawa na wale wa nchi zingine” —Profesa Mkenda