Naibu wa Rais wa zamani Nchini Kenya Kalonzo Musyoka amesisitiza suala la mshikamano katika Jumuiya ya Afrika mashariki hasa kuusu suala la sarafu moja ya Jumuiya hiyo ili kuweza kufungua milango ya kiuchumi.
Musyoka ameyazungumza hayo katika makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa zoezi la kuwaapisha wabunge wapya wa bunge hilo
Amesema kuwa kuwepo kwa nchi ya Congo kunapelekea msukumo mkubwa wa kiuchumi katika Nchi za Afrika Mashariki na kuwataka wabunge wa EAC kufanya kazi ya kuziungani nchi zote na kufungua mipaka ili isiwe na vikwazo na wananchi wa nchi hizo wawe na usawa na uhuru wa kibiashara.
“Tulifanya kazi kubwa sana kuurudisha umoja huu wa Afrika mashariki kuipata Jumiya hii mpya baada ya Jumuiya hii kuvunjika mwaka 1977 lakini baadaye viongozi wetu wa nchi Kutoka Tanzania wakati ule alikuwa ni Benjamin Mkapa, Mwai kibaki pamoja na Museven na badae tuliweza kutoa ripoti yetu kwa Mawaziri na hadi leo mnapoiona leo Jumuiya ilipo fika”. Alieleza Musyoka.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, amewasihi wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuendeleza mtangamano ili kukuza biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Dkt Tax ameeleza kuwa suala la umoja ni muhimu kwani lazima kwenda pamoja katika sekta mbalimbali hususani programu za kuendeleza miundombinu inayoakisi uchumi wa kijiografia kwa nchi wanachama wa EAC.