Mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka sekondari ya kimataifa ya International School of Tanganyika(IST), Madeleine Kimaro amechangisha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kutoa huduma za mazoezi tiba kwa wanafunzi wasiopungua 15 katika Kituo cha Msimbazi Mseto Ilala kitengo cha Usonji kwa muda wa mwaka mmoja.
Inaelezwa kuwa Mradi huo utashirikisha wataalamu wa mazoezi ambao watakuwa wakifanya kazi mda wote pia watakuwa wakiwapatia wanafunzi chakula cha mchana hapo shuleni na kutoa usafiri wa kuwafata nyumbani kuwaleta shule na kuwarudisha nyumbani kwa muda wa mwaka mmoja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Afisa Elimu Maalumu Mkoa wa Dar es salaam, Swalehe Msechu amesema kuwa Serikali inaendelea kuandaa mazingira wezeshi kwaajili ya kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu ikiwemo watoto wenye usonji huku akitoa wito kwa jamii kuacha imani potofu kuhusu watoto wenye usonji.
Aidha ametoa wito kwa wazazi na wanafunzi wote kuwapeleka watoto wenye mahitaji maalumu shuleni ili waweze kupata huduma muhimu na kuacha mila potofu na kuwaficha ndani watoto hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Faundation, Hilda Nkabe amesema mradi huo utawasaidia watoto katika mazoez tiba ya mawasiliano na mazoezi tiba kazi.